News and Events June 2011
The CCT Executive Council Declaration
JUMUIYA YA KIKRISTO TANZANIA CCT
MKUTANO WA HALMASHAURI KUU WA 45
TAMKO
Katika kikao chake cha kawaida cha Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) kilichokaa katika Kituo cha Mikutano na Mafunzo (CCT-CTC) mjini Dodoma tarehe 1 – 2 Juni, 2011 wajumbe walikaa na kutafakari wajibu wa Kanisa wa kitume na kinabii kwa taifa letu. Wajumbe wanamshukuru Mungu na kuwapongeza wananchi wote kwa kuweza kupita salama katika mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana 2010. Wanampongeza Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuchaguliwa kwake mara ya pili kuiongoza nchi yetu. Aidha wanaipongeza pia Serikali kwa kuweza kusimamia Uchaguzi huo hadi kuwapata viongozi walioko madarakani sasa. Ni vyema sasa vyama vyote vya siasa vielekeze juhudi zao zote katika kutafuta kuwahamasisha wananchi kujiletea maendeleo licha ya tofauti zao za kiitikadi na kisiasa. Aidha wajumbe wanampongeza Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujasiri wake wa kukubali kuridhia matakwa ya wananchi walio wengi ya kutaka kuandikwa kwa Katiba Mpya. Dira kubwa iwe kuleta maendeleo ya kweli kwa taifa letu yanayozingatia amani, demokrasia, usawa na umoja wa kitaifa. Pamoja na haya Jumuiya inapenda kutamka baadhi ya mambo muhimu kama ifuatavyo hapa chini:
1. Mungu anachukia dhambi
Viongozi wote wenye dhamana ya kuwaongoza wananchi hawana budi kutambua kwamba Mungu anachukia dhambi na huchukia wote wanaoifanyia dhambi mzaha. Maovu yanayotajwa kila siku ikiwa ni pamoja na rushwa, ufisadi na uporaji wa raslimali za taifa letu yasifanyiwe mzaha ili kuepusha kuleta maangamizi kwa raia wema wasio na hatia. Viongozi waepuke kutoa kauli zenye maneno matamu yenye lengo la kuwapotosha wananchi ili wapate ridhaa yao na baadaye waingie madarakani na kujinufaisha na kusahau ahadi zao. Waepuke kauli zenye kuwachanganya wananchi na kuleta migogoro.2. Mauaji ya raia
Yametokea matukio kadhaa ya mauaji ya raia katika sehemu kadhaa nchini mwetu. Baadhi yalitokea mwaka jana katika kipindi cha kampeni za Uchaguzi Mkuu na siku za karibuni. Kumwagika kwa damu ya Watanzania hawa siyo ishara nzuri. Mauaji ya namna hii hata kama yatafanywa na raia au vyombo vya Dola hayakubaliki. Ikumbukwe kwamba mwanadamu ameumbwa kwa mfano wa Mungu, hivyo ni vibaya kujichukulia sheria mkononi kinyume na makusudi ya Mungu na sheria za nchi.3. Migogoro ya kidini
Kumekuwa na matukio ya viashiria vya machafuko miongoni mwa makundi ya imani mbalimbali nchini kwetu. Matukio haya ni pamoja na mihadhara ya dini kutoa kashfa dhidi ya dini nyingine. Mahali pengine kumekuwa na uvamizi wa jinai wa kuchoma moto majengo ya ibada na kuwajeruhi waumini na hata kusababisha vifo kama vile huko Mto wa Mbu mkoani Arusha. Hali hii ni ya kutisha na haikutazamiwa kutokea miongoni mwa dini. Wito unatolewa kwa makundi yote ya Imani kumwogopa Mungu na kuheshimu haki na uhuru wa kila mwananchi kuamini dini na kufanya ibada anayoitaka pasipo kuvunja haki na uhuru wa wananchi wenzake. Hali hii ikiendelea italitosa Taifa katika vita kama tunavyosikia huko Somalia na kwingineko. Vita ya namna hii itawaathiri wanyonge na wasio na hatia.4. Siku za ibada
Siku za ibada kwa dini zote hazina budi kuheshimiwa na watu wote na mamlaka zote. Ni vyema Serikali isipange matukio muhimu ya kitaifa kama vile Uchaguzi Mkuu na chaguzi za Serikali za Mitaa siku za Ibada yaani Jumapili.5. Siku za ibada vyuoni
Kadhalika wahadhiri na wakufunzi wa Vyuo Vikuu, vya elimu ya juu na taasisi zake wasiwapangie wanafunzi mitihani au mazoezi ya vitendo siku za ibada.6. Hali ya uchumi
Licha ya Serikali kutangaza kwamba hali ya uchumi nchini imekua, hali ya wananchi walio wengi imeendelea kuwa ngumu. Bei za bidhaa kama vile mafuta ya kuendeshea magari na mitambo na huduma mbalimbali hususan gharama za kusomesha watoto katika shule na vyuo, gharama za umeme, madawa ya binadamu na ya mifugo zimepanda sana wakati kipato cha wananchi wengi kimeshuka au kimebaki palepale. Kadhalika hatima ya wanafunzi katika Vyuo vikuu na vya elimu ya juu kuhusu kupewa mikopo imekuwa si ya kueleweka. Ufa kati ya wananchi wa kawaida na wale wenye nacho unazidi kupanuka na kuibua matabaka. Hali hii inasababisha malalamiko miongoni mwa wananchi dhidi ya Serikali yetu. Malalamishi na ukweli huu umechukuliwa na wadau wa vyama vya siasa kufanya maandamano ambayo yamekuwa yakiwavutia wananchi wengi. Hali hii inachangia hali ya kisiasa kuwa tete hasa ikilinganishwa na baadhi ya nchi jirani ambapo bei ya mafuta iko chini sana zaidi ya hapa nchini na nchi hizo zinapitisha mafuta yao hapa nchini katika barabara zetu. Serikali isahihishe jambo hili pasipo kulichelewesha.7. Katiba Mpya
Mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya ni jambo ambalo Serikali haina budi kulisimamia na kuwaelimisha wananchi wote kwa usahihi na kwa makini sana. Ukusanyaji wa maoni ya wananchi na makundi yote ya kijamii na hatimaye kuandikwa na kuridhiwa kwa Katiba Mpya hauna budi kufanywa na chombo huru. Kazi hii isiharakishwe na wala isicheleweshwe. Yafaa iwe imekamilika mapema ndani ya muda wa kadri kabla ya kuanza kwa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.8. Uharibifu wa mazingira
Wajibu wa kutunza mazingira ya nchi yetu umo mikononi mwa wananchi wa Tanzania. Tunao wajibu wa kuwa mawakili wema wa mazingira yetu ili kuhifadhi na kulinda uoto wetu wa asili na mbegu endelevu. Huko nyuma mwaka 2006 CCT iliitahadharisha Serikali dhidi ya uingizwaji wa mbegu za viini tete (GMO) na kuitaka isitishe kabisa zoezi la kutengeneza sera ya matumizi ya mbegu hizi. Walakini kwa siri na bila kuwashirikisha wananchi wa maeneo husika na hasa wakulima wadogowadogo serikali imeruhusu kufanyika kwa majaribio ya mbegu hizi. Hali hii imesababisha malalamiko miongoni mwa wakulima wadogowadogo wakionyesha hofu yao kuwa mbegu za asili zitatoweka na pia kwamba hawataweza kumudu gharama za kununua mbegu na kuyatunza mashamba ambapo mbegu hizo zimepandwa. Hali hii ni ya hatari itakayotufanya kuwa na kilimo kisicho endelevu bali tegemezi na vituo vyetu vya utafiti wa mbegu asilia hapa nchini vitafungwa. Serikali inaombwa kutofumbia macho rai hii na kusitisha kabisa mpango huu.9. Uvunaji wa mali asili
Uwekezaji katika uvunaji wa maliasili za madini, uvuvi, utalii, uwindaji na kilimo umeendelea kutowasaidia watanzania. Badala yake wananchi wa maeneo husika wamejikuta ni wageni katika maeneo yao ya asili na kuzungukwa na doria. Hawawezi tena kufanya kazi za kujikimu katika maeneo hayo na kuonekana kama wezi na wavamizi. Matokeo yake mahali pengi yamekuwa ni wananchi kuteswa hadi kuuawa kama kule Nyamongo Wilaya ya Tarime (mfano wa hivi karibuni) ambapo wananchi watano waliuawa na Polisi. Isitoshe katika maeneo ya migodi kuna uchafuzi wa mazingira katika maeneo yanayoizunguka na kusababisha madhara katika afya kwa wananchi na mifugo. Huko Loliondo wananchi wamenyanyaswa na mwekezaji wa uwindaji ambapo nyumba na vyakula vya wananchi vilichomwa moto na kuwafanya kuwa wakimbizi katika nchi yao. Serikali haina budi kusitisha mikataba hiyo iliyofanywa pasipo kuwashirikisha wananchi kwelikweli na kuweka mazingira mazuri na ya haki yatakayowanufaisha wananchi na Serikali zao kwanza pasipo unyanyasaji, mauaji na unyonyaji. Kadhalika Serikali isimamie na kuhakikisha kwamba Hati Miliki za Vijiji kwa wananchi zinapatikana kwa gharama nafuu na mapema iwezekanavyo.10. Kutoa uraia kwa wakimbizi kisirisiri
Ziko taarifa za kuaminika kwamba Serikali imekwisha kuwapatia maeneo ya makazi ya kudumu raia kutoka nchi jirani ya Burundi waliokuwa wakiishi hapa wakiwa wakimbizi. Jambo hili ni jema lakini Serikali haina budi kujiridhisha kwamba wananchi asilia wa maeneo husika wanashirikishwa kikamilifu ili matakwa yao ya msingi yakidhiwe kwanza. Itakuwa ni uchokozi endapo mamlaka yoyote itatekeleza jambo hili kwa siri pasipo kuzingatia rai hii. Mtindo wa Serikali wa kutekeleza mambo kisirisiri hususan yale yanayogusa maslahi ya wananchi kama vile umilikaji ardhi, uvuvi, uchimbaji madini, utalii na uwindaji na matumizi ya kodi ya wananchi haukubaliki kwa watanzania. Wananchi wa maeneo husika hawana budi kuulizwa ni mchango wao kuheshimiwa.11. Tiba asilia
Tiba asilia imeonekana kupendwa na wananchi wengi nchini na kutoka nje ya nchi kama vile Tiba ya Mchungaji Mstaafu wa KKKT Ambilikile Mwasapile. Kadhalika Chuo Kikuu cha Afya na Tiba cha Muhimbili na taasisi mbalimbali zimekuwa zikizifanyia tafiti mbali mbali tiba hizi. Manufaa ya tiba hizi ni pamoja na kuwa zinapatikana kwa bei nafuu na ni asilia zinaweza kupatikana muda wote. Tunatoa wito kwa Serikali kutoa ushirikiano zaidi kwa wadau hawa na matokeo ya utafiti yawekwe bayana ili kuwaondolea wananchi hofu na ili huduma zitakazothibitishwa zipatikane mahali pengi nchini. Kadhalika serikali isimamie utunzaji wa mazingira ili miti na mimea mingine yenye vyanzo vya tiba asili isitawi na kupatikana muda wote.12. Mahakama ya kadhi
Jumuiya ya Kikristo Tanzania inarudia na kusisitiza msimamo wake kwamba mambo ya kuendesha shughuli za kidini yatenganishwe na shughuli za mamlaka ya kuendesha nchi. Kuanzisha Mahakama ya Kadhi nchini ni jambo zuri linalowahusu waislamu. Kwa kuwa ni jambo la kidini waachiwe waislamu wenyewe pasipo kutumia hazina ya Serikali ambayo ni fedha ya walipa kodi wote nchini.MUNGU IBARIKI TANZANIA
MUNGU IBARIKI AFRIKA
Askofu Peter Kitula
MWENYEKITI WA CCT
DAR ES SALAAM
6 JUNI, 2011